Wajasiriamali nchini watakiwa kujiamini

Wajasiriamali nchini watakiwa kujiamini

422
0
SHARE

Na Grace Ndossa

WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kujiamini kwa kila wanachofanya ili kuongeza ufanisi na mafanikio katika biashara zao.
Mwito huo umetolewa na Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Mhandisi Emmanuel Ole Naiko na mlezi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Diana Women Empowerment Organisation jana jijini Dar es Salaam.
Alikuwa akikutana na Kamati ya Utendaji ya taasisi hiyo na Kampuni ya China Direct inayotoa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali.
“Mjasiriamali anatakiwa kujua anachokifanya na kujiamini,” alisema Balozi Ole Naiko. Aliiomba Kampuni ya China
Direct kufikisha ujuzi na mawazo waliyonayo kwa Watanzania wengi ili waweze kunufaika na elimu hiyo.
Alisema ujasiriamali si kitu rahisi kama wengi wanavyodhani, bali ni suala linalotakiwa kuzingatiwa kielimu na umakini.
“Ujasiriamali ni kazi, ujasiriamali ni elimu Watanzania waelewe kuwa bila kupata elimu huwezi kufika pale
unapopahitaji,” aliongeza.
Aliwataka Watanzania kuhudhuria mafunzo ya ujasiriamali kila wanapopata fursa na nafasi, kwani bila hivyo biashara wanazoanzisha hazitakuwa na mafanikio yanayotarajiwa.
“Wajasiriamali watenge muda kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ili kuongeza nafasi ya mafanikio,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa China Direct, Tunu Cheka, aliwaomba Watanzania kujiunga katika vikundi mbalimbali vya ushirika kama vile taasisi ya Diana Women Empowerment Organization ili waweze kuunganishwa katika mtandao wa ujasiriamali na kufanya biashara kwa wepesi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Taifa wa Diana Women Empowerment Organization, Farida Khakoo, aliwaomba wanachama wa taasisi
hiyo kujituma na kujiamini katika yale wanayoyafanya na mwisho wa siku watapata mafanikio.
“Tatizo la wanachama wangu wanakosa kujiamini, nawaomba mjiamini, kwani kujiamini ni ndiyo msingi wa mafanikio katika jambo lolote,” alisema Khakoo.