kitaifa

Magufuli ajitosa jipu udahili TCU

Friday, June 3 2016, 0 : 0

 

RAIS Dkt. John Magufuli, amempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kwa hatua alizochukua ili kusafisha idara zilizo chini ya Wizara yake ili kutoa elimu bora.

Alisema Serikali yake itahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo lakini haitakubali kuelekeza mikopo hiyo kwa wanafunzi wasio na sifa za kujiunga na Vyuo Vikuu.

Dkt. Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Awali Dkt. Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa chuoni hapo inayojengwa katika Kampasi ya Mlimani Mashariki mwa chuo hicho.

Akiwahutubia maelfu ya wanajumuiya hiyo wakiwemo wanafunzi, Wahadhiri na wafanyakazi wa chuo, Dkt. Magufuli alisema Serikali yake imedhamiria kutoa elimu bora kwa Watanzania na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto zinazovikabili vyuo.

Alieleza kusikitishwa kwake na uwepo wa wanafunzi waliodahiliwa katika baadhi ya vyuo nchini pasipo kuwa na sifa zinazomwezesha kujiunga na chuo kikuu.

"Wapo wanaokopeshwa mikopo ya elimu ya juu lakini hawana sifa, unakuta mwanafunzi ana D,D lakini anasajiliwa na kuchukua digrii Chuo Kikuu, kupata mkopo wa Serikali hii ni aibu ya ajabu.

"Haiwezekani, wakati tunawalipia wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na kupata D,D wangine wakiwa na divisheni 4 inasikitisha, wapo wanafunzi wa kidato cha sita wamekosa mikopo, wengine wana diploma nao wamekosa mikopo," alisema Dkt. Magufuli.

Wanafunzi na siasa

Katika hatua nyingine, Dkt. Magufuli aliwataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini, kuacha kujihusisha na masuala ya siasa badala yake wazingatie jukumu lililowapeleka vyuoni ambalo ni kusoma ambapo Serikali yake haitavumilia vitendo vya vurugu vyuoni.

"Ifike mahali Watanzania tukubali ukweli, tuache siasa katika masuala ya msingi, ukimpeleka mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye ufaulu wa divisheni 4 kuchukua digrii, akishatoka pale hata kama atafanikiwa kupata digrii itakuwa ni ajabu.

"Niwaombe wanafunzi wote, msitumiwe na wanasiasa, mmekuja kusoma, someni, siasa mtazikuta mkiondoka ndiyo maana hata katika kutoa mikopo hatubagui, sijui huyu CCM au yule CHADEMA, wote ni Watanzania, ndiyo lengo letu," alifafanua Dkt. Magufuli.

Aliongeza kuwa; "Nashukuru ambao hamjagoma,kuweni na subira wakati Serikali inaposhughulikia mambo yenu, mikopo ni haki yenu, hata mimi hadi hapa nilipofika nilisaidiwa," alisema.

Aliahidi kuwa, Serikali yake itahakikisha inatoa mahitaji ya wanafunzi ikiwemo mikopo, kuboresha miundombinu ya vyuo, kuwataka wanavyuo kuwa wavumilivu, wazalendo pale ambapo mahitaji hayo yatachelewa kutokana na mchakato wa kuyapata kuhitaji muda.

Aahidi kuchangia bil. 10/-

Kabla ya kuhutubia wanajumuiya hao, Mkuu wa chuo hicho Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, alimuomba Dkt.Magufuli asaidie kuboresha miundombinu chuoni hapo, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ambao asilimia 70 wanaishi nje ya chuo.

Kutokana na ombi hilo, Dkt. Magufuli aliahidi kutoa sh. bilioni 10 na kuuagiza uongozi wa chuo hicho kuainisha eneo ndani ya chuo ili ujenzi wa mabweni hayo uanze mara moja.

Dkt. Magufuli alisema chuo hicho kina eneo kubwa ambalo halina kazi hivyo wahakikishe wanajenga mabweni chuoni hapo si nje ya eneo hilo kama ilivyo sasa kwani zaidi ya 4000 wanaishi nje.

"Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo, jengeni mabweni haraka, mimi nitatafuta sh. bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi huo, kuanzia sasa tangazeni tenda ili Mkandarasi apatikane na kuanza ujenzi," alisema.

Alishangazwa kuona chuo hicho kikiwa na eneo kubwa lisilo na mabweni kwa ajili ya wanafunzi badala yake wanafunzi 3,000 ndiyo wanaokaa katika mabweni ya chuo.

Aliitaka Mifuko ya Hifadhi za Jamii nchini, kuwekeza kwenye ujenzi wa mabweni katika vyuo mbalimbali kikiwemo UDSM badala ya kujenga nyumba za makazi ambazo wakati mwingine hazikaliwi na watu.

Alisema nyumba nyingi zinajengwa na mifuko hiyo, nyingine hazikaliwi na watu hivyo alihoji kwanini wasijenge mabweni ya wanafunzi ambao wanauhakika na lazima wakae katika nyumba hizo.

Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kumpongeza Profesa Yunus Mgaya kwa uzalendo, moyo alionao kwa Taifa lake akimuhakikishia kuwa, mbali na kuondolewa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), atampa nafasi nyingine kama hiyo.

"Jamani mimi ndiyo Rais, nakuahidi Prof. Mgaya wewe ni mzalendo kwani watu walitaka kukuchafua lakini umeonesha kutubu, kuwaasa watu waiache TCU ifanye kazi yake, nitakupa kazi nyingine, wewe ni mzalendo na Mtanzania wa kweli," alisema Dkt. Magufuli.

Uzinduzi wa ujenzi wa maktaba hiyo ya kisasa, ulihudhuriwa na Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing, ambaye nchi yake ndiyo imechangia dola za Marekani zaidi ya milioni 41 za ujenzi huo.

Maktaba hiyo ya kisasa itakapokamilika, itakuwa ndiyo bora kuliko zote barani Afrika ikiwa na ukubwa wa eneo la mita za mraba 20,000, uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja.

Sakata la TCU

Mei, mwaka huu, Prof. Ndalichako, aliivunja Bodi ya TCU kutokana na kudahili wanafunzi 486 wasio na sifa Chuo Kikuu cha St. Joseph.

Mbali ya kuvunja bodi hiyo, aliwatumbua jipu kwa kuwasimamisha kazi Maofisa waandamizi wa TCU kwa kushindwa kusimamia, kutekeleza wajibu wao.

Waliosimamishwa ni pamoja na Prof. Mgaya kwa kushindwa kusimamia shughuli za TCU na wajibu wake kama Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo.

Wengine waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Ithibati, Rose Kiishweko aliyekuwa Mkurugenzi wa Udahili, Kimboka Instambuli na kusisitiza haiwezekani mwanafunzi mwenye D-4 awe na sifa za kusomea digrii.

"Haiwezekani wasio na sifa wapewe mikopo na wenye nazo wakose, hii ni sawa na wafanyakazi hewa,"í alisema na kumteua Profesa Eleuther Mwageni kukaimu nafasi ya Katibu Mtendaji wa TCU.

Prof. Ndalichako pia alimteua Dkt. Kokubelwa Mollel, kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Udahili na Nyaraka na kuongeza kuwa, wanafunzi 424 waliokuwa wakisoma St. Joseph wametafutiwa vyuo vingine.

Alisema baada ya wanafunzi hao kujiunga na vyuo hivyo, walionekana wapo nyuma katika masomo kwa tofauti ya mwaka mmoja ambapo wale waliopelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambao St Joseph walikuwa mwaka wa tatu, walirudishwa nyuma mwaka mmoja.

Aliongeza kuwa, waliotoka Tawi la Songea kuhamia Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), walionekana na udhaifu katika masomo yao hali iliyoufanya uongozi wa chuo hicho kuwapa masomo ya ziada.

Bunge lajitosa mauaji ya Tanga

Thursday, June 2 2016, 0 : 0

 

MATUKIO ya mauaji yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini sasa yamegusa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo limetaka serikali kuwasilisha taarifa ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria kuhusiana na mauaji hayo.

Uamuzi huo umetangazwa bungeni jana mjini Dodoma na Naibu Spika wa Bunge, Dkt.Tulia Ackson, ambapo ameitaka Serikali kuwasilisha taarifa kuhusu mauaji hayo.

Dkt. Tulia alitangaza uamuzi huo mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

" Nimepata taarifa ya Serikali kwamba Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamad Masauni,yuko safarini mkoani Tanga kufuatilia mauaji yaliyotokea hivyo serikali ilete majibu ya mauaji hayo.

"Pamoja na taarifa ya Naibu Waziri kuwepo safarini namtaka alete taarifa kwa sababu Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo hapa na Waziri anayehusika na mambo ya Bunge naomba watuletee taarifa kwa sababu mauaji yamekuwa yakitokea mara nyingi na tumekuwa tukiisihi Serikali ituletee taarifa; nahisi mtakuwa mnazitafuta," alifafanua Dkt. Tulia.

Aliitaka Serikali kuwasilisha taarifa hiyo mbele ya Bunge haraka, kwani Bunge linahitaji kujua nini kinaendelea na Bunge lijiridhishe na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.

Mbali ya kauli hiyo ya Naibu Spika, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kwa tiketi ya CCM, Kangi Lugola, aliomba mwongozo akitumia kanuni 68,7 na akisema:

"Kutokana na mauaji yanayotokea nchini nimelazimika kuomba mwongozo huu kwa sababu matukio ya mauaji yaliyoanza kujitokeza ni mengine. Mambo haya tuliwahi kuuliza serikali na ikaahidi kutoa ufafanuzi."

Waheshimiwa wabunge mambo haya tulishaiomba Serikali iyafanyie kazi na kutuletea taarifa;ni jinsi gani inajipanga kukabiliana nayo, lakini kutuambia leo kwamba naibu waziri amekwenda kushughulikia jambo hili wakati huo huo mambo ambayo yametokea Mwanza na maeneo mengine tulishaitaka Serikali itueleze kinachotokea.

Tuambie ina mikakati ya kukabiliana na mambo haya ambayo tunaamini ni sehemu ya ugaidi,wale waliofanya mauaji Tanga jana waliweza kunyang'anya vyakula wakarudi navyo kwenye mapango ya Amboni hizi ni dalili tosha kama haya ni mauaji ya ugaidi kwa sababu magaidi ishara mojawapo ni kuvizia watu na kuwanyang'anya vyakula au kuwaua na kurudi sehemu zao ili waendelee kufanya mauaji.

Sasa Mhesimiwa Naibu Spika tutaendelea kukaa katika hii hali ya kuambiwa Naibu waziri ameenda Tanga na matokeo yake atakaporudi wanaendelea kukaa kimya na mauaji yanaendelea kutokea."

Akijibu mwongozi huo Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu) ,Jenista Mhagama, alisema Serikali inajua kwamba mauaji haya yanawagusa Watanzania wote.

Alisema kwenye tatizo hilo ambalo limejitokeza mara kadhaa sasa katika nchi yetu, Naibu Spika umesema ni vema Mheshmiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wanaohusika na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alishakwenda Mwanza na tangu jana yupo Tanga.

"Si kwamba ni jambo jepesi la kusimama tu kama Serikali na kutoa taarifa kwa mambo haya yanayotokea bila kuyafuatilia," alisema.

Alisema si sahihi kwa mauaji hayo ambayo yametokea kuanza kusema tu ni mauaji ambayo yanafanana na ugaidi na kwamba mauaji yamekuwa yakitokea na Serikali imekuwa ikiwakamata majambazi mbao wamekuwa wakifanya mambo hayo.

"Serikali tuachiwe kufanya kazi hiyo kama tulivyokuwa tunaanza kufanya na pale tutakapoona tumejiridhisha na taarifa makini kwa maagizo ambayo waziri mkuu ataweza kuyafanyia kazi tutaweza kuyatolea taarifa ambayo itaeleweka kwa Watanzania," alisema.

 • RC avunja ukimya uhalifu Tanga

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

   

  MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella, amesema matukio ya uhalifu yaliyojitokeza mkoani humo ni tishio kwa maendeleo ya wananchi na Mkoa kwani yanaweza kufukuza wawekezaji.

  Shigella aliyasema hayo jana baada ya kupokea taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Esterina Kilasi, kabla ya kuhudhuria Baraza Maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

  Baraza hilo lilikuwa likijadili hoja za halmashauri zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

  Alisema uhalifu huo unaleta sura mbaya kwa Mkoa ambao unatarajia kufikiwa na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga.

  "Uhalifu huu unaweza kuwajengea hofu wawekezaji waliopo Tanga, hakuna mwekezaji anayependa kuwekeza sehemu ambayo si salama kwani mwisho wa siku akajikuta anapigwa risasi au kuhamisha mali zake ndani ya muda mfupi," alisema.

  Aliongeza kuwa, jukumu la ulinzi linapaswa kuwa chini ya wananchi wenyewe ambao ndiyo wanaowajua wahalifu, kuishi nao, wakat i mwingine wananchi huwasaidia wahalifu kutoroka.

  "Vita hii ni tofauti na vita ya askari wanaorushiana risasi bali inaweza kumpita adui yako njiani, baadhi ya wananchi hutoa taarifa kwa wahalifu na kupewa pesa au vocha za simu...wahalifu huelezwa polisi wako njiani na wao hukimbia," alisema.

  Shigella alisema uhalifu pia unaweza kupunguza fursa za kiuchumi katika Mkoa huo ambao una fursa nyingi ikiwemo bandari, reli, barabara na sasa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda ambalo litakuwa na faida kubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

  Alisisitiza kuwa , wanaofanya uhalifu huo si magaidi bali wameamua kuharibu uchumi wa Mkoa, kuwatia hofu wananchi ambao aliwataka wasiwe na hofu yoyote kwani Tanga iko salama na viongozi wote wakiwemo wakuu wa vyombo vya ulinzi, usalama, wamejipanga kupambana na watu hao wakishirikiana na wananchi.

  "Hapa hakuna Al- Shabaab wala Al-Qaeda, hawa ni maadui zetu wanaotaka kurudisha nyuma maendeleo ya Mkoa," alisema.

  Hadi sasa ndani ya miezi mitatu, watu 13 wamefariki dunia mkoani humo kutokana na matukio mbalimbali ya uhalifu likiwemo tukio la Aprili 20, mwaka huu, ambapo watu watano waliuawa kwa risasi baada ya majambazi kuvamia duka la Central Bakery.

  Majambazi hao pia walipora fedha taslimu sh. milioni 2.7 ambapo mwanzoni mwa Mei, mwaka huu, majambazi walivamia Kitongoji cha Kibatini, kuchinja kuku 40, mbuzi wawili na ng'ombe mmoja.

  Mwishoni mwa wiki, majambazi waliua watu wanane kwa mapanga katika Mtaa wa Kibatini, Kata ya Mleni, kuiba mchele, biskuti na kutokomea kusikojulikana.

  Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, waliouawa katika tukio hilo ni Issan Hussein, Mkola Hussein, Mikidadi Hassan, Issa Ramadhani na wengine wawili walifahamika kwa jina moja moja la Kadir na Mahamudu.

 • Waangalizi EU: NEC, ZEC hazikuonesha uwazi

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

   

  UJUMBE wa Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), jana umewasilisha ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25,2015 na kubainisha kasoro zinazopaswa kurekebishwa ili zisiweze kujirudia katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

  Mbali ya kubaini kasoro hizo, waangalizi hao walisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), hazikuonesha uwazi kamili juu ya michakato yao ya kufanya maamuzi.

  Ripoti hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na mwangalizi Mkuu ambaye ni Mbunge wa Bunge la Umoja wa Jumuiya ya Ulaya, Judith Sergentini ambaye alisema waangalizi kutoka zaidi ya nchi 28, walikuwepo nchini tangu mwanzo wa kampeni hadi siku ya utoaji matokeo wakiwa 14.

  Akizungumzia uchaguzi huo, alisema kuwa pamoja na kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kushirikisha vyama vingi vya siasa, Serikali inapaswa kuchukua hatua kadhaa ili kuboresha uchaguzi ujao kuwa huru zaidi.

  Alisema suala la mgombea binafsi linapaswa kuzingatiwa katika chaguzi zote za Muungano na Zanzibar, kuwa na haki ya kudumu kwa vyama vya siasa kuunda umoja wao nyakati za uchaguzi.

  Waangalizi hao wameshauri sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015 kuangaliwa upya ili uchaguzi uweze kuwa wazi na wananchi waweze kupata taarifa zaidi za uchaguzi.

  Sergentini alisema ipo haja ya NEC kufanya marekebisho juu ya upatikanaji wa Makamishna wake katika uteuzi ili kuongeza imani juu ya uhuru wao.

  Aliongeza kuwa, maamuzi ya NEC yasiwe sauti ya mwisho badala yake matokeo ya Rais yaruhusiwe kuhojiwa mahakamani ili kuondoa dosari mbalimbali, kuzifanya pande zote zilizoshiriki kujiridhisha.

  Waangalizi hao walipendekeza NEC iweze kufungua ofisi kwenye ngazi za mikoa na Wilaya ili kurahisisha usimamizi wa uchaguzi.

  Kufutwa matokeo Z'bar

  Akizungumzia matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyofutwa na ZEC, Sergentini alisema EU na waangalizi wengine wa kimataifa, walielezea wasiwasi wao katika tamko lao na kuiomba ZEC iwasilishe ushahidi wa kuhalalisha uamuzi huo ambao haujawahi kutokea.

  Alisema ushahidi huo haujawahi kuwasilishwa hivyo EU na waangalizi wengine wa kimataifa, hawakufanya uangalizi katika Uchaguzi wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi 20, mwaka huu kwa kuwa iliona mazingira hayakuwa na uchaguzi shirikishi, halisi na kuaminika.

  Alipendekeza upatikanaji wa Makamishna wa ZEC, uangaliwe upya ili kujenga Demokrasia na uwazi nyakati za chaguzi, kuangaliwa upya mchakato wa uandikishwaji wapigakura Zanzibar.

  "Ninafurahi kuwasilisha ripoti yetu leo kwa kuwa inajumuisha yote tuliyoyaona wakati wa uangalizi kwa kipindi cha miezi mitatu ambacho ujumbe ulikuwepo nchini na kutoa mapendekezo yetu," alisema.

  Aliongeza kuwa , umoja huo unaendelea kusimamia dhamira yake ya kufanya kazi na washirika wake Tanzania ili kuimarisha mchakato wa kidemokrasia nchini, kutazama kwa karibu marekebisho yote.

  "Ripoti inatoa mapendekezo muhimu ya kufikiriwa na mamlaka husika, taasisi za usimamizi wa uchaguzi na wadau wengine wa uchaguzi," alisisitiza Sergentini.

 • Upinzani wawatibua wabunge CCM

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  UAMUZI wa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson, wakidai kutokuwa na imani naye umewatibua wabunge wa CCM.

  Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, wabunge wa CCM walihoji sababu ya uongozi wa Bunge kuendelea kuwalipa posho wabunge wa kambi hiyo bila kufanya kazi bungeni badala yake wamekuwa wakiingia, kusaini na kuondoka.

  Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe, alilazimika kuomba mwongozo wa Naibu Spika akitumia Kanuni ya 68 (7), akitaka kujua sababu ya wabunge hao kulipwa posho, wakati kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Katiba ya nchi.

  Alisema Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inasema kila mtu ana wajibu wa kuitii Katiba na ibara ya 2, kila mtu ana haki ya kufuata utaratibu uliowekwa na sheria.

  "Hivi ndivyo ninavyofanya hapa, naomba mwongozo huu kwa sababu ya matakwa ya sheria... pia nasimama kama Waziri kuhakikisha nchi inazingatia utawala wa sheria kwa kutumia ibara ya 23 (1).

  "Ibara hii inamtaka kila mtu bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote, kupata ujira unaolingana na kazi yake, watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao, watapata malipo kutokana na sifa za kazi wanazozifanya," alisema.

  Dkt. Mwakyembe aliongeza kuwa, kitendo cha wabunge wa upinzani kuingia bungeni, kukaa muda mchache, kuondoka na kulipwa posho bila kufanya kazi hakiwezi kukubalika hivyo aliomba mwongozo kama wabunge hao ambao wamejiondoa kwa ridhaa yao na kwenda kupumzika kama wanastahili kulipwa posho.

  Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku, aliomba mwongozo na kudai suala alilozungumza Dkt. Mwakyembe aliwahi kulisemea bungeni lakini kiti cha Spika kimekuwa kikitoa majibu ya kuahidi kulitolea majibu lakini hakijafanya hivyo hadi sasa.

  Aliongeza kuwa, ipo haja ya suala hilo kupelekwa kwenye Kamati ya Kanuni ili iweze kufanya maamuzi kwani kiti cha Spika kimeshindwa kulitolea maamuzi badala ya wabunge hao kuingia bungeni, kutoka lakini bado wanasaini posho.

  "Ni muhimu sana kuwepo kanuni za kuwabana wabunge ambao wamesimamishwa kushiriki vikao vya Bunge ili wasiweze kufanya shughuli zozote katika majimbo yao ikiwemo mikutano ili kutoa fundisho kwa wabunge waliobaki bungeni wasivunje kanuni zilizopo kwa makusudi," alisema.

  Juzi mbunge wa Nkasi Kaskazini, Alli Keissy, naye aliomba mwongozo akidai wabunge wa kambi hiyo wamekuwa wakiingia bungeni, kusaini na kutoka jambo ambalo wanaiibia Serikali, kitendo hicho hakikubaliki.

  Kutokana na hoja hizo, Dkt. Ackson, alisema suala la wabunge ambao walisimamishwa lakini wameendelea kulipwa nusu mshahara na posho, atalifikisha katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ndiyo imewawajibisha ili iweze kufafanua adhabu hiyo na matumizi ya kifungu namba 75.

 • Makonda ampa pikipiki 'bodaboda' aliyepambana na majambazi Dar

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa zawadi ya pikipiki ambayo thamani yake ni zaidi ya sh. milioni mbili kwa mwendesha bodaboda aliyepambana na majambazi waliokuwa na silaha na kufanikisha kukamatwa.

  Makonda alitoa zawadi hiyo Dar es Salaam jana kwa mwendesha bodaboda, Stephen Gerald, mkazi wa Magomeni, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi aliyopigwa na majambazi hao.

  Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hiyo yenye namba za usajili MC 307 BDR, aina ya Boxer, Makonda alisema tukio hilo limemgusa alipoliona katika vyombo vya habari na kumtafuta kijana huyo.

  Alisema kitendo alichokifanya kijana huyo ni cha kupongezwa kwani kama angekuwa katika nchi zingine, angekuwa shujaa kutokana na ujasiri wake wa kuweka maisha yake rehani.

  "Nimeguswa na tukio hili, mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, nimelazimika kukupa zawadi hii ili kuunga mkono jitihada zako, pamoja na kupigwa risasi lakini ulihakikisha majambzi hayo yanakamatwa hivyo wewe ni mfano wa kuigwa," alisema Makonda wakati akikabidhi pikipiki hiyo.

  Aliongeza kuwa, suala la ulinzi na usalama ni la kila mtu hivyo Wenyeviti wote wa Serikali ya Mtaa, wahakikishe wanahakiki wakazi waliopo maeneo yao ili kuwabaini wageni.

  "Ni muhimu pia wapangaji wakihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, wapate kibali cha Mwenyekiti wa Mtaa aliohama na akifika eneo lingine akikabidhi kibali chake ili ajulikane," alisema Makonda.

  Akizungumzia tukio hilo, Gerald alisema yeye alilazimika kuwafukuza majambazi hao ambao walikuwa na pikipiki mbili, kuingia kati yao na kuwagonga mbali ya kuwa na bastola.

  "Sisi bodaboda mara nyingi tunakosa wateja kwa sababu ya watu wachache kutumia pikipiki kufanya uhalifu, ilikuwa siku ya Jumapili, kuna dada mmoja aliibiwa na majambazi ambao walipita barabarani wakipigiwa kelele za wezi ndipo nilipowasha pikipiki yangu na kuwafukuza," alisema.

  Alisema aliwafukuza hadi eneo la Extenal ambapo majambazi hao waliingia katika barabara ya vumbi ndipo akawagonga kwa makusudi hivyo waliruka na kuziacha pikipiki zao chini.

  "Baada ya kuruka, mmoja kati ya majambazi hao alitoa bastola na kabla ya kuipiga, nilimsukuma akapoteza mweleko nikamrukia na kudondoka naye chini, wakati nahangaika naye alinipiga risasi mgongoni nikaishiwa nguvu.

  "Alitokea mwanajeshi mmoja aliyekuwa na bastola na kupiga juu risasi mbili akiwataka watu wote waliokuwa wanashuhudia tukio hilo walale chini," alisema Gerald na kuongeza kuwa, majambazi hao walimpiga risasi nyingine ambayo ilimkosa na kutoboa pikipiki yake aina ya Boxer namba MC 629 AGB.

  Aliliomba Jeshi la Polisi nchini kuwa karibu na waendesha bodaboda ili waweze kusaidia katika suala zima la ulinzi na usalama, kuwadhibiti wezi na majambazi wanaotumia pikipiki kufanya uhalifu.

  Katika hatua nyingine, Makonda ameiomba Serikali ya China kupitia Jeshi la Majini nchini humo, kulipatia Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam boti tatu za doria ili kudhibiti uhalifu wa baharini.

  Makonda alitoa ombi hilo Dar es Salaam juzi katika hafla ya kupokea meli tatu za Jeshi la China zilizokuwa zikilinda ghuba ya Aden mwambao wa Somalia ili kuwadhibiti maharamia wanaoteka meli za mizigo.

  Alisema kuja kwa meli hizo zenye wanajeshi zaidi ya 200 ni kutokana na uhusiano mzuri kati ya Serikali ya Tanzania na China ambazo uhusiano huo ulianzishwa na waasisi wa mataifa hayo.

  "Kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli na Serikali ikiwemo ya Mkoa wa Dar es Salaam, tunawashukuru kwa kufika hapa lakini namuomba Kamanda wa Meli hizi tatu atusaidie nasi tupate hata boti tatu za doria kwa Jeshi letu la Polisi ili tukomeshe vitendo vya magendo ambavyo

  vinaikosesha Serikali mapato kwa kuingia bidhaa feki, dawa za kulevya na wahamiaji haramu," alisema Makonda.

kimataifa

Bomu laua watu 10 na kujeruhi 60-Somalia

Friday, June 3 2016, 0 : 0

 

 

MAAFISA wa Usalama nchini Somalia wamesema watu zaidi ya 10 wameuwawa baada ya kundi la itikadi kali la Al Shabab kuizingira hoteli maarufu mjini Mogadishu na kufanya mashambulizi yaliyomalizika jana asubuhi.

Miongoni mwa waliouwawa ni wabunge wawili pamoja na walinzi wa usalama ambapo watu wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa.

Mshambuliaji wa kujitoa mhanga ndani ya gari aliendisha gari hadi katika lango la Hoteli iliyojulikana kwa jina la Ambassador ambayo inapendwa na maafisa wa Serikali na wafanyabiashara jioni ya jana iliyopo katikati ya mji Mkuu Mogadishu.

Mlipuko uliotokea uliosababishwa na shambulizi hilo la kujitoa mhanga na kuharibu lango kuu la kuingia Hoteli hiyo ambalo linaulinzi mkali na kuharibu pia maduka yaliyoko karibu na Hoteli hiyo.

Mapema jana asubuhi vikosi vya usalama viliwauwa watu watatu waliokuwa na bunduki waliokuwa wamejificha ndani ya Hoteli hiyo hatua iliyofikisha mwisho wa hujuma za Al shabab zilizochukua muda wa zaidi ya masaa 10 dhidi ya hoteli hiyo.

Rais Hassan Sheikh Mahamoud alilaani kitendo hicho cha kigaidi.

Tumbaku inaweza kuua watu bilioni moja-UN

Thursday, June 2 2016, 0 : 0

 

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) , Ban Ki- Moon, amesema ana wasiwasi na ongezeko la idadi ya vifo vinavyosababishwa na matumizi ya tumbaku duniani.

Katika taarifa yake aliyoitoa juzi katika maadhimisho ya Siku ya Dunia bila ya Tumbaku inayoadhimishwa Mei 31 ya kila mwaka, Ban alisema kuwa sigara na bidhaa nyinginezo za tumbaku zinatoa roho za watu milioni 6.6 kila mwaka.

Katika taarifa yake hiyo, Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa udhibiti wa tumbaku ni jambo la lazima ili kufikia malengo ya maendeleo ya dunia na kuonya kwamba endapo hazitafanyika jitihada zaidi katika suala hilo huenda tumbaku ikaua watu wanaofikia bilioni moja katika karne hii.

Alisema mbali na vifo hivyo, lakini pia wengine hufariki kutokana na athari za moshi wa wavutaji sigara.

Ki-Moon alisema kuwa Siku ya Dunia bila ya Tumbaku iliadhimishwa katika wakati ambapo viwanda vya sigara vinachukua hatua zaidi za kudhoofisha jitihada za kupunguza madhara ya tumbaku duniani.

Ban alifafanua kuwa sigara na bidhaa za tumbaku zinakwamisha maendeleo na kuzidisha umaskini kwa kuzingatia kuwa ni watu maskini ndiyo wanaovuta sigara zaidi na kuathirika zaidi kwa kubeba mzigo wa madhara ya kiuchumi na maradhi yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku.

 • Mwanamke aliyekataa kuolewa auawa kwa moto Pakistan

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  MWANAMKE mmoja nchini Pakistan amechomwa moto hadi kufa baada ya kukataa wito wa ndoa ya mtoto wa bosi wake.

  Mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Maria Sadaqat ambaye ni Mwalimu wa shule aliye na umri mdogo alishambulia nyumbani kwake na kundi moja la wanaume siku ya jumapili na kufariki katika hospitali mjini Islamabad siku ya Jumatano.

  Familia yake ilisema kuwa alikataa kuolewa na mtoto wa mmiliki wa shule ambayo alikuwa akifundisha.

  Wanaharakati wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake walisema kuwa visa vya mashambulio dhidi ya wanawake wanaokataa kuolewa ni vingi nchini Pakistan.

  Kiongozi wa jimbo la Punjab Shahbaz Sharif alianzisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo.

  Baba wa msichana huyo alisema kuwa mmiliki wa shule hiyo ni mojawapo ya watu waliomshambulia mwanaye.

  Polisi wal i liambia Shi rika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba wanaume hao walimpiga kabla ya kumwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto karibu na eneo la kitalii la Muree,lililopo Karibu na mji Mkuu wa nchi hiyo Islamabad.

 • Wafanyakazi waliogoma wakata umeme-Ufaransa

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  WAFANYAKAZI waliogoma nchini Ufaransa wamelitumbukiza gizani eneo la Magharibi mwa nchi hiyo baada ya kukata umeme unaoelekea upande huo na kuzikalia njia za usafiri wa treni katika kituo Kikuu cha reli mjini Paris jana.

  Tukilo limetokea wakati Vyama vya Wafanyakazi wa Viwanda vya Nyuklia na Shirika la Taifa la huduma za Reli wakigomea mapendekezo ya kufutwa kwa baadhi ya Sheria za Ulinzi wa ajira.

  Wafanyakazi hao wanadai mambo mbalimbali yaliyokuwa yanahusiana na sekta zao,lakini pia walitumia fursa ya hasira zilizosambaa dhidi ya muswada wa serikali wa kurefusha muda wa kazi wa masaa 35 kwa wiki na kurahisha mchakato wa kuajiri na kufukuza wafanyakazi.

  Wanachama wa Chama cha CGT katika viwanda 16 kati ya 19 vya nyuklia nchini Ufaransa, ambavyo vinasambaza umeme kwa sehemu kubwa zaidi ya nchi, walipiga kura kugoma kwa siku moja jana.

  Wafanyakazi wa Kiwanda cha Brittany walikata umeme katika eneo la Saint-Malo-de-Guersac, na kusababisha ukosefu wa huduma hiyo muhimu kwa kaya zisizopungua 120,000 kulingana na mtandao wa umeme wa TRE.

 • Opec washindwa kufikia makubaliano

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  NCHI zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) zimeshindwa kuafikia juu ya ukomo wa uzalishaji wa mafuta kama baadhi ya nchi wanachama wa Shirika hilo walivyotaka.

  Mawaziri wa nchi hizo walikutana nchini Australia kujadili mambo mbalimbali juu ya OPEC ikiwemo pendekezo la Saudi Arabia kutaka kuwepo na kiwango maalumu cha uzalishaji wa mafuta.

  Hata hivyo nchi hizo zilishindwa kufikia makubaliano ya juu ya mpango uliopendekezwa na Saudi Arabia wa kutaka paweko ukomo wa uzalishaji mafuta ili kuimarisha soko la biashara ya bidhaa hiyo duniani.

  Mbali na kushindwa huko lakini pia OPEC ilifikia uamuzi wa kumchagua Mohammed Barkindo afisa anayehusika na suala la Mafuta nchini Nigeria kuwa Kiongozi wake mpya wa shirika hilo.

  Barkindo ambaye ataanza rasmi majukumu yake katika OPEC kwa kipindi cha miaka mitano mnamo mwezi Agosti ni mtu anayetajwa kuwa na ujuzi wa muda mrefu katika sekta ya mafuta.

  Aliwahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Shirika hilo mnamo mwaka 2006.

  Mkutano wa mjini Vienna wa mawaziri wa mafuta kutoka nchi za OPEC ulikumbwa na migawanyiko kuhusu suala la kuwekwa viwango vya uzalishaji wa bidhaa hiyo.

 • Human Rights Watch wataka kukomeshwa unyonyaji vibarua

  Thursday, June 2 2016, 0 : 0

   

   

  SHIRIKA la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, wametaka kukomeshwa mara moja unyonyaji unaofanywa dhidi ya wafanyakazi ambao ni vibarua duniani.

  Mkurugenzi Shirika hilo kitengo cha haki za Watoto Juliane Kippenberg,alitoa ripoti hiyo sambamba na kuanza kwa Mkutano wa kimataifa wa kazi huko mjini Geneva, Uswisi.

  Alisema kuna haja ya kuwepo makubaliano mapya ya kimataifa ya kuyalazimisha mashirika na makampuni yaache kuwatumikisha watoto wadogo na kuendeleza utumwa mamboleo kwa ajili ya kudhamini masilahi yao.

  Kippenberg alifafanua katika ripoti yake hiyo kwamba wengi miongoni mwa wafanyakazi hao ambao ni vibarua ni wale watengenezaji wa nguo watoto wanaofanyishwa kazi kwenye mashamba ya tumbaku, wachimba migodi.

  Alisema ni wale vibarua katika miradi ya ujenzi ambao wamekuwa wakitumiwa vibaya na hakuna njia na taratibu za kuwawezesha kufikisha malalamiko yao wala mawakili wa kuwatetea.

  Kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa na Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO) lililo chini ya Umoja wa Mataifa, watu wapatao milioni 21 wanafanyishwa kazi kwa nguvu katika pembe mbalimbali duniani.

biashara na uchumi

Standard Chartered kinara kwa huduma bora nchini

Thursday, June 2 2016, 0 : 0

 

BENKI ya Standard Chartered Tanzania imeshinda tuzo ya huduma bora kwa wateja iliyotolewa kwa benki iliyoweza kutoa huduma bora kwa wateja ambapo, ushindi huo ulitangazwa wakati wa chakula cha jioni, wiki iliyopita jijini Nairobi, Kenya.

Tuzo kwa benki za Afrika 'The Africa Banker Awards' ina lengo la kubainisha na kuzipa tuzo benki zinazofanya vizuri katika huduma za kibenki kwa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu tuzo hiyo ilitokana na kura zaidi ya 23,500 zilizpigwa na jamii inayopata huduma za kibenki katika nchi za Afrika mashariki.

Akizungumza wakati wa kupokea tuzo hiyo Mtendaji mkuu wa benki hiyo, Sanjay Rughani, alisema kuwa kwanza anawashukuru wateja na wadau mbalimbali wa benki hiyo katika nchi za Afrika Mashariki kuipigia kura za kuiamini benki hiyo kwa utendaji bora.

Aliongeza kuwa benki hiyo imeelekeza nguvu zake zaidi kwa huduma kwa wateja na baadhi ya mikakati imeshaanza kuchukuliwa kwa kuwaeleza wafanyakazi wa benki hiyo katika mikutano yao kuhusu matarajio ya wateja.

"Wafanyakazi wetu wamepata mafunzo mbalimbali na tumetambua kuwa uwekezaji wetu katika mafunzo hayo kwa uboreshaji huduma kwa wateja yameleta matokeo chanya na kutupa washindi kwa kutoa huduma bora kwa wateja nchini Tanzania," alisema Rughani.

Aidha, alibainisha kuwa wataendelea kutoa huduma bora kwa huduma mbalimbali za benki kwa kuendelea kuwekeza zaidi katika mitandao ya simu ya kibenki kwa kurahisisha huduma kwani wameongeza huduma hizi kwa mitandao ya M-PESA na TigoPesa kwa shughuli za miamala.

Kwa upande wake mtendaji wa huduma za kifedha Robin Amlot alisema kuwa watahakikisha wanalinda ubora wa utendaji wa kazi bora na wanawashirikisha wadau wao kuwa na matokeo yenye ubora kwa kuboresha uchumi katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Alisema kuwa ushindi wa tuzo hiyo unamulika mawazo ya wateja juu ya sekta ya huduma za kifedha katika eneo hili la Afrika Mashariki na ushindi huo unaweza kuwa ni sifa kwa mafanikio waliofikia.

Ushirika Lokolova wapata mafanikio

Wednesday, June 1 2016, 0 : 0

 

CHAMA cha Ushirika cha Lokolova kilichopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kimepata sura mpya baada ya juzi kusaini mkataba na Kampuni ya Interconsult Limited ya kufanya kazi ya usanifu wa mji wa kisasa utakaokuwa chini ya ushirika huo.

Mkataba huo ulisainiwa kati ya uongozi wa ushirika huo na ule kampuni ya Interconsult, katika hafla iliyofanyika katika mji wa Himo, Wilaya ya Moshi.

Akiongea muda mfupi baada ya kusainiwa mkataba huo, mwenyekiti wa ushirika huo, Samuel Sam, alisema tukio hilo ni hatua kubwa itakayofunika makovu yaliyopatikana kufuatia vikwazo ambavyo vilijitokeza na kuathiri ushirika huo kwa miaka kadhaa.

"Ilifikia wakati ushirika wetu ukatangazwa kufutwa lakini busara ya Kaimu mrajis wa vyama ushirika nchini, Dkt. Audax Rutabanzibwa ukatunusuru ushir ika wetu ukarudishwa," alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wanachama wa ushirika huo kuendelea kuunganisha nguvu zao katika kuhakikisha mafanikio yaliyoanza kuonekana yanakuwa ya manufaa kwa ushirika huo na wanachama wake.

Kwa upande wake mshauri wa kisheria wa ushirika huo wakili Eliakunda Kipoko, alitoa rai kwa uongozi wa ushirika huo na wanachama wake kushikamana ili mafanikio yaliyopatikana yalenge kukua.

"Sasa kazi ndiyo imeanza,kuna wenye nia njema ambao watawaunga mkono katika hatua yenu hii mpya, lakini pia mjihadhari kwani wasiowatakia mema watatafuta mbinu mpya za kutaka kuzuia msiende mbele, njia ya kuwashinda hawa ni nyie kumwomba Mwenyezi Mungu na kushirikiana kwa pamoja," alisema.

 • Aliyenufaika Airtel Fursa ampa zawadi Mkurugenzi Mkuu Airtel

  Thursday, June 2 2016, 0 : 0

   

  KUPITIA kampeni ya Airtel Fursa ambayo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa vijana nchini kuwawezesha kufanikisha ndoto zao, mmoja kati ya vijana wanaojihusisha na ubunifu wa sanaa za uchoraji aliyenufaika na mradi huo, Theresia Maliatabu, jana alimtembelea Mkurugenzi Mkuu wa Airtel na kumkabidhi picha yake aliyoichora mara tu baada ya Airtel Fursa kumpatia vifaa vya kidigital.

  Kijana huyo alinufaika katika semina iliyofanyika miezi miwili iliyopita ambapo iliwachagua vijana wawili walioweza kuwezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi katika semina hiyo kwa ajili ya kuboresha ubunifu wao.

  Akikabidhi zawadi hiyo Theresia alisema: "Vifaa hivyo vinanisaidia kubuni baadhi ya michoro ambayo ni ya kisasa zaidi,lakini hasa inanisaidia mazoezi katika kuchora na vile vile inanisaida kama sehemu ya kutangaza biashara yangu."

  "Napenda kuwaambia vijana wenzangu kwamba wajiamini na vipaji walivyokuwa nazo wasikate tamaa kwani kila kitu kinawezekana na wasiache kuchangamkia fursa kama hizi zinapojitokeza," aliongeza Theresia.

  Mpaka sasa Airtel imefanya semina nyingi sana za mafunzo ya biashara ya ujasiriamli hapa nchini katika mikoa mbalimbali na kuweza kufikia vijana wapatao 4,000. Airtel kupitia mpango wake wa Airtel FURSA utaendelea kutoa warsha hizi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuhakikisha inafikia vijana wengi zaidi.

  Vijana wanahamasishwa wanaposikia nafasi kama hii popote walipo, kuchangamkia kwa kuhudhuria kwani elimu inayotolewa ni bure kabisa bila gharama yoyote.

 • Vijiji 50 kunufaika na Mradi wa REA

  Thursday, June 2 2016, 0 : 0

   

  JUMLA ya vijiji 50 vya Wilaya ya Mpwapwa mkoni Dodoma vitanufaika na mpango wa mradi wa umeme vijijini ujulikanao kama REA awamu ya tatu utakaoitwa Underline Program.

  Hayo yalibainishwa na meneja wa Shirika la Umeme la (TANESCO) wilayani hapa, Theodory Hall, ofisini kwake alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.

  Theodory alisema kuwa vijiji vitakavyonufaika na mpango huo ni vile vijiji vilivyo pitiwa na miundombinu ya umeme lakini vijiji hivyo havikuwa kwenye mpango wa kupata umeme japo kuwa miundombinu ya umeme ulipita katika eneo hilo.

  "Mradi huu utaitwa underline; ni mradi ambao umelenga kuvipatia huduma vijiji vile ambavyo miundombinu ilipita hapo lakini havikuwa na huduma hiyo hilo lilileta malalamiko mengi kwa vijiji hivyo na baadhi ya watu ambao walikuwa si waungwana walidiriki kuharibu hata miundombinu ya umeme," alisema Hall.

  Aidha, Bw.Hall alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi na wadau wote wa TANESCO kushiriki na kutoa taarifa za vitendo vya watu ambao wanahujumu miundombinu ya TANESCO kwa ajili ya matumizi yao binafsi.

  Hall alisema wananchi wanaweza kutumia mitandao kijamii kama facebook,twiter na Istagram na kila atakayetoa taarifa atapewa kiasi cha fedha kutokana na ukweli wa taarifa yake.

 • Dar Brew yazindua mwonekano mpya wa Chibuku Super

  Wednesday, June 1 2016, 0 : 0

   

  KAMPUNI ya Dar Brew jana ilizindua chupa mpya ya bia ya asili ya Chibuku Super yenye ujazo wa milimita 750, ambayo mtumiaji halazimiki kurudisha chupa pale anapoitumia.

  Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa Dar Brew, Oscar Shelukindo alisema, bia hiyo iliyopo katika chupa nzuri ya plastiki inayovutia, itauzwa kwa bei ya sh. 1,000 tu kwa kila chupa.

  "Leo (jana) ni siku ya furaha kubwa sana kwetu Dar Brew na kwa watumiaji wote wa bia, kwani tumefanikiwa kuzindua chupa hii itakayouzwa kwa bei nzuri ya Sh 1,000 tu na kwa ujazo unaotosheleza.

  "Bia hii imetengenezwa kwa utaalamu wa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ya kisasa kabisa, hivyo tunawahakikishia watumiaji ubora wa hali ya juu," alisema.

  Shelukindo alisema, bia hiyo imetengenezwa kwa kutumia malighafi za hapa nyumbani, ikiwemo nafaka ya mtama ulio bora, hivyo kuna kila sababu kwa Watanzania kujivunia kilicho chao na kukumbuka asili yao, kwani hii ni bia yao ya asili.

  "Chibuku Super ina kilevi cha asilimia 4, kinachokufanya uitumie kwa muda mrefu ukiwa na marafiki, lakini inakupa lishe nzuri kutokana na virutubisho vinavyopatikana katika nafaka zilizotumika kutengeneza bia hii," alisema.

  Naye Meneja Mauzo na Usambazaji wa Dar Brew, Fred Kazindogo alisema, bia hiyo itaanza kupatikana nchi nzima katika baa, maduka makubwa (Super Markets), katika maduka ya jumla na rejareja na sehemu zinazouzwa vileo kuanzia leo.

  "Tunatarajia wateja na wapenzi wa bia wataifurahia chupa hii mpya na kwa wauzaji wa jumla, tunaamini watahamasika kuuza Chibuku Super kwani ina faida nzuri na haina usumbufu wa kununua chupa," alisema.

  Kazindogo alisema, ana imani kubwa wapenzi wa bia wataipokea kwa shangwe na wataitumia ili kuonesha wanajali asili yao.

 • Fastjet yatangaza shindano kwa wateja

  Wednesday, June 1 2016, 0 : 0

   

  SHIRIKA la ndege za bei nafuu Afrika, Fastjet, limefanya ndoto za usafiri kuwa za kweli kwa abiria wake zaidi ya milioni mbili barani Afrika tangu kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2012 kwa kuanzisha shindano kwa wateja wake.

  Hatua hiyo ni kama mkakati wa kuhamasisha hata Watanzania wengi zaidi kusafiri; Fastjet imetangaza kwamba abiria yeyote anayenunua tiketi tangu mwisho wa mwezi wa Mei ataingia kwenye bahati nasibu ya kwanza ya aina yake ijulikanayo 'Big 10 draw' ambapo washindi 10 watasafiri bure katika njia yoyote ya Fastjet katika mtandao wake barani Afrika.

  Kwa watu kumi watakaoshinda bahati nasibu hiyo shirika linawapa uwezo wa kwenda katika mapumziko au kwenda katika safari ya manunuzi pamoja na marafiki na familia suala ambalo walikuwa wakiliwazia muda mrefu.

  Ama kwa wajasiriamali wa Tanzania, safari hiyo inaweza kutumia kukuza mahitaji ya biashara kwa kuokoa gharama za usafiri katika safari nyingine kumi wanazozihitaji kusafiri.

  "Ni rahisi, lengo la Fastjet ni kufanya uwezekano kwa wateja wengi kusafiri, iwe ni kwa shughuli za biashara, kutembelea marafiki na familia, au kufurahia burudani ya kusafiri," alisema Meneja Mkuu wa Fastjet Tanzania John Corse.

  Njia ambazo zinahusiana kwa ajili hiyo ni safari za kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, Mwanza,Kilimanjaro, Zanzibar, Nairobi, Entebbe, Lusaka, Harare na Johannesburg; halikadhalika safari kati ya Kilimanjaro na Harare.

  Tiketi zitakazonunuliwa Mei 31, mwaka huu kwa njia za kimataifa na za ndani zitawawezesha abiria wake kuingia katika bahati nasibu ya Big 10.Washindi watatangazwa Juni 2016 na safari 10 za bure ni lazima zifanyike kabla ya Desemba 11 mwaka huu.

  Ikitambuliwa kama shirika la ndege la gharama nafuu Afrika,Fastjet hivi sasa inafanya safari ndani ya nchi 11 kwa wafanyabiashara,watalii na familia ambazo zimeipokea tozo lake la nauli nafuu na linalofikia kwa usafiri wa anga.

michezo na burudani

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU YANGA: manji aibua mapya

Friday, June 3 2016, 0 : 0

 

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amechukua fomu rasmi ya kutetea nafasi yake ndani ya klabu hiyo, ikiwa na kutoa shutuma zake kwa baadhi ya viongozi wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baadhi ya wanachama wake ambao wanataka kuhujumu uchaguzi huo.

Mbali na Manji kutetea nafasi yake pia Makamu Mwenyekiti wake Clement Sanga naye amechukua fomu ya kutetea nafasi yake.

Manji amechukua fomu kogombea nafasi hiyo kwa lengo la kuendeleza jitihada za maendeleo ndani ya klabu.

Wakati wa kuchukua fomu, Manji hakusita kuzungumzia sakata la uchaguzi mkuu, huku akimvua uanachama Mohammed Msumi baada ya kudaiwa kufanya njama na TFF, pamoja na watendaji wa BMT kwa lengo la kuhujumu uchaguzi wa klabu hiyo.

Mbali na Msumi, Manji pia amewasimamisha uanachama wale wote waliochukua fomu za kugombea Yanga kupitia TFF hadi suala lao litakapojadiliwa na Kamati ya Nidhamu.

Manji ambaye alionekana kuwa na jazba na kuwasikilizisha wanachama wa Yanga sauti zilizorekodiwa zikisikika kupanga njama hizo za kuhujumu uchaguzi.

Sauti hizo zilizosikika kupitia gari la matangazo, zilikuwa zikibishana juu ya nini kifanyike ili kuhakikisha wanamuondoa Manji katika uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wanachama wa klabu hiyo, Manji alisema kuwa anawashangaa viongozi wa TFF kusema kuwa wao hawataki kufanya uchaguzi jambo ambalo si kweli.

Alisema, tangu mwaka jana walitaka kufanya uchaguzi lakini TFF waliwaandikia barua na kutaka wasitishe hadi baada ya kupita uchaguzi mkuu wa nchi.

Alisema walikubaliana na suala hilo na kuamua kusogeza mbele, lakini mwezi Januari wakiwa katika harakati hizo Alex Mngongolwa alifiwa na baba yake na kuamua kusimamisha mchakato ule.

Kinachomshangaza zaidi ni madai ya TFF kuwa hawautambui uongozi wao wakati wapo pale kwa ajili ya wanachama waliowaomba kuongeza mwaka mmoja.

"Wakati wa mkutano wetu mkuu uliofanyikia ukumbi wa Polisi wanachama wote walikuja na hoja na kutuongezea mwaka mmoja ili kukamilisha baadhi ya mambo ndiyo tuingie kwenye uchaguzi mkuu," alisema Manji.

Alisema TFF wanatakiwa kutambua kuwa uchaguzi wa Yanga haupo kwa ajili ya maslahi binafsi bali upo kwa ajili ya maslahi na maendeleo ya klabu yao.

Akizungumzia juu ya katiba ya klabu hiyo, Manji alisema kuwa baada ya katiba yao ya mwaka 2010 kuonekana na upungufu waliambiwa wafanye marekebisho na kuongeza baadhi ya kamati.

Marekebisho hayo yalihusisha kuongezeka kwa kamati ya nidhamu pamoja na maadili na walifanya hivyo na kuirudisha TFF.

"Kama TFF walitutaka tufanye marekebisho nasi tukafanya na leo wanasema uchaguzi utatumia katiba ya zamani inamaana hawakusajili katiba yetu," alisema Manji.

Alisema wanashindwa kuelewa lengo hasa la TFF na BMT kwa klabu yao ni nini, kwani mara nyingi wamekuwa na vikwazo visivyo na maana na vinaonekana wazi vinalengo la kuua timu yao.

Manji alisema kuwa TFF wamekuwa wakiwafanyia mchezo mchafu na kutaka kuwadidimiza kiuchumi jambo ambalo wamelifanikisha kwa kiasi fulani.

"TFF wametuingiza katika mikataba inayotunyonya kama klabu, pia wamekuwa wakitufanyia mambo mengi yasiyofaa pia hamuwezi kuamini kuwa hadi leo zawadi zetu za kombe la FA bado hatujakabidhiwa," alisema Manji.

Aidha Manji alimuagiza Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Jerry Muro kupeleka ushahidi huo kwa vyombo vya dola ili viweze kufanyiwa kazi.

"Ushahidi huu utapelekwa polisi na TAKUKURU ili kuwachukulia hatua wahusika, pia Muro atakuwa akifuatilia kila wiki ili kutoa taarifa kwa umma na kutambua nini kinaendelea juu wa watu hawa," alisema.

Kwa upande wao TFF kupitia kwa Msemaji wake Alfred Lucas alisema kuwa Shirikisho litatoa tamko rasmi juu ya uchaguzi huo Juni 8, mwaka huu.

Alisema kuelekea katika uchaguzi huo anawaomba wanachama na wapenzi wa Yanga waendelee kuwa watulivu ili kulinda amani iliyopo.

Yanga yataja wanaohujumu uchaguzi wao

Thursday, June 2 2016, 0 : 0

 

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema umebaini mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya watu ili kutaka kuvuruga uchaguzi wao.

Lawama hizo zimetupwa moja kwa moja kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, viongozi wa Serikali pamoja na watendaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Yanga si wa kwanza kutupa lawama kwa TFF, kwani ni juzi tu Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) , alielekeza lawama zake kwa mmoja wa watendaji wa shirikisho hilo.

Kinacholalamikiwa zaidi kwa mtendaji huyo ni kuchelewesha kwa makusudi zoezi zima la uchukuaji fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro alisema kuwa wanashangazwa na kitendo cha baadhi ya watendaji hao kutaka kuwahujumu.

Alisema, kwa bahati mbaya hujuma hizo zimegonga mwamba, kwani uchaguzi wao utafanyika na tayari wana ushahidi wa kutosha juu ya watu hao.

Jerry alisema kuwa tayari wana ushahidi wa sauti na video unaoonesha mipango ya kuharibu uchaguzi wa klabu yao.

"Tunawajua watu wanaotaka kuvuruga klabu yetu na tuna ushahidi wa sauti na video unaoonesha vile vyote walivyokuwa wanavipanga," alisema Muro.

Alisema, wanachokisubiri sasa ni kuukamilisha ushahidi huo na kuuweka hadharani ili watu wabaini hujuma wanazofanyiwa.

Muro aliwataka watu hao wasithubutu kuendelea kuingilia uchaguzi wao na endapo wataendelea na vitendo hivyo wataonja joto ya jiwe.

 • Azam Academy wawapa kichapo Future Stars

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC (Azam Academy) juzi ilianza vyema michuano ya 'Azam Youth Cup 2016', baada ya kuinyuka Future Stars Academy kutoka Arusha kwa mabao 4-1.

  Mchezo huo uliofanyika jioni ndio ulikuwa wa ufunguzi wa michuano hiyo inayofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, nje kidogo ya Dar es Salaam kabla ya kushuhudiwa Ligi Ndogo Academy kutoka nchini Kenya wakiwachapa Football for Good Academy (Uganda) mabao 2-1.

  Azam Academy iliuanza vyema mchezo huo kwa kuonesha uhai mkubwa kipindi cha kwanza na ndani ya dakika 37 tu, ikaweza kujipatia mabao yote manne kabla ya Future Stars kuwabana kipindi cha pili kwa kuwazuia wapinzani wao wasipate mabao zaidi.

  Iliwachukua dakika 17 tu, Azam Academy kuweza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Shaaban Idd aliyemtoka kipa wa Furure Stars, Elias Lembris, kabla ya kufunga bao hilo, dakika moja baadaye Rajabu Odasi akaongeza bao la pili.

  Future Stars ilikuja juu mara baada ya kupata bao la kwanza dakika 25 lililofungwa na Nazir Abdul kwa kichwa, lakini nguvu zao zilinyongíonyeshwa kufuatia Shaaban tena kuipatia bao la tatu Azam Academy dakika ya 28 akitumia vyema pasi safi ya nahodha Abdallah Masoud ëCabayeí.

  Odasi aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa katika eneo la kiungo akishirikiana vema na Masoud, alipigilia msumari wa mwisho kwenye lango la Future Stars kwa kuipatia bao la nne Azam Academy kwa shuti zuri akiunganisha krosi iliyochongwa na Ramadhan Mohamed.

  Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam Academy ilienda kifua mbele kwa mabao hayo, hata iliporejea kipindi cha pili ilishindwa kuongeza mabao mengine kufuatia Future Stars kuubana uwanja.

  Hata hivyo kipa wa Future Stars Elias, anastahili pongezi kubwa kufuatia kuokoa michomo mingi ya wapinzani wao kipindi cha pili, baadhi ikipigwa na Optatus Lupekenya dakika ya 62 na Yahaya Zaidi dakika ya 72.

  Kikosi hicho kinachonolewa na Tom Legg kutoka nchini Uingereza na Msaidizi wake, Idd Cheche kilimaliza mchezo huo kwa ushindi huo mnono na kufanya wafikishe jumla ya pointi tatu wakiwa juu ya Ligi Ndogo ambao walipata ushindi finyu wa mabao 2-1 dhidi ya Football for Good.

  Mchezo huo wa pili ulikuwa mkali na wa aina yake kwa timu zote kugawana vipindi, Football for Good wakimiliki kipindi cha kwanza na Ligi Ndogo wakingíara zaidi kipindi cha pili.

  Ligi Ndogo ilibidi itoke nyuma baada ya kutanguliwa kufungwa bao dakika ya 39 na Otim Oradiga na kurejea mchezo kwa mabao mawili ya ushindi yaliyopigwa na Eric Kivuva.

  Michuano hiyo jana ilikuwa kwenye mapumziko na itaendelea tena leo, mchezo wa kwanza utakaoanza saa 10.00 jioni utakuwa kati ya Future Stars na Ligi Ndogo huku Azam Academy ikimenyana na Football for Good saa 1.00 usiku.

 • Timu ya Alliance yasaka wapya 13

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  KITUO cha Kulea na Kukuza Vipaji cha Michezo cha Alliance Schools Sports Academy (ASSA), kinatarajia kuzindua mpango maalumu wa kukiboresha kikosi cha timu yake ya Alliance Football Club (AFC) inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2016/2017.

  Kikosi hicho kinahitaji wasakata kabumbu 13 watakaoungana na wachezaji waliopo ambao waliiwezesha kupanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2016/ 2017.

  Mkurugenzi wa kituo hicho, James Bwire akizungumza na waandishi wa habari jana kituoni hapo alisema programu hiyo itakayofahamika kwa jina Alliance Maboresho 2016 ilizinduliwa juzi kwa kuwafanyia usaili vijana waliojitokeza kwenye zoezi hilo linalosimamiwa na makocha wa kituo hicho.

  Alisema vijana wa kiume wenye uwezo na vipaji vya kucheza soka wa umri wa miaka 18 hadi 25 kutoka mikoa yote ya Tanzania wajitokeze kwenye usaili utakafaonyika katika kituo hicho ambapo ulianza jana hadi kesho kuanzia asubuhi.

  Alieleza kuwa baada ya usaili Mei 30 hadi Juni 3 , mwaka huu kutachezwa mechi mbalimbali zikiwahusisha vijana watakaofuzu kwenye usaili huo kwa ajili ya kuibua na kupata vipaji bora na vijana watakaochaguliwa na jopo la makocha wa kituo hicho watasajiliwa na kujiunga moja kwa moja na timu ya Alliance Football Club (AFC) pamoja na kituo cha Alliance School Sports Academy.

  Mkurugenzi huyo ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mwanza aliongeza kuwa lengo la program hiyo ni kuibua vipaji vya vijana waliosahaulika waweze kuonesha uwezo wao, lakini waliokwisha kutumikia vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu, Darala la Kwanza na la Pili hawatakuwa na nafasi kwenye usaili huo.

  Tunahitaji kupata vijana 13 kwa ajili ya kukiboresha kikosi chetu na wenye majina hatuwahitaji. Tunataka kuwapa nafasi vijana ambao hawajaonekana wa umri wa miaka 18 hadi 25.Usaili utafanyika katika kituo chetu kilichopo kwenye Kata ya Mahina wilayani Nyamagana,î alisema Bwire.

  Alieleza kuwa Alliance Academy inendelea kuamini kuwa pamoja na ubora wa kikosi chao bado kuna vijana wengi wenye uwezo kisoka, ambao hawajapata nafasi ya kucheza soka kwenye timu kama hiyo ya Aliiance Football.

  Alliance Academy ina timu za vijana wa umri mbalimbali kuanzia umri wa miaka 11 hadi 17 wanaolelewa kwenye kituo hicho, ambapo pia kinahudumia vijana wenye vipaji wa timu ya vijana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 • Mourinho: Guardiola hanipi tabu

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  KOCHA Jose Mourinho amesema kamwe hatathubutu kupoteza muda wake kumwangalia Pep Guardiola pekee kwenye ligi ya England msimu ujao, kwasababu anaamini akifanya hivyo, basi ataruhusu timu nyingine kuchukua ubingwa.

  Mourinho, ambaye aliteuliwa kocha wa Manchester United wiki iliyopita anakabiliwa na mtihani mgumu mbeleni kutokana na uwepo wa hasimu wake mkubwa Pep Guardiola ambaye atakuwa akiinoa Manchester City ambao ni mahasimu wakubwa wa Manchester United.

  Ikumbukwe tu vita ya Guardiola na Mourinho ilianza nchini Hispania wakati huo Mourinho akiinoa Real Madrid na Guardiola akiinoa FC Barcelona.

  Licha ya uhasimu mkubwa walionao kutokana na historia yao, Mourinho amesisitiza kwamba hataendekeza jambo hilo katika maisha yake mapya ya ukocha katika klabu ya Manchester United.

  Akiongea wakati akiwa Lisbon University, Mourinho alisema: “Uzoefu wangu hauniruhusu mimi kuwa innocent (mtu asiye na hatia).

  “Nilikuwa na Guardiola kwa miaka miwili La Liga ambapo ilikuwa ama mimi au yeye ndiyo tulikuwa tuna nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa. Lakini hapa kama nikisema nimwangalie tu yeye, basi timu nyingine zitanipiku na kuchukua ubingwa”.

 • Argentina yatishia kujitoa Copa America

  Friday, June 3 2016, 0 : 0

   

  CHAMA cha soka nchini Argentina (AFA) kimetishia kuitoa timu yake ya taifa nje ya mashindano ya Copa America kutokana na serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya soka.

  Argentina ni miongoni mwa timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kuibuka bingwa wa michuano hiyo itakayofanyika Marekani na Juni 7 wanatarajia kucheza mchezo wao wa kwanza dhidi ya mabingwa watetezi Chile kwenye mji wa Santa Clara, Califonia.

  Lakini ushiriki wao umeingia mashaka baada ya AFA kuingia kwenye mgogoro na serikali ya Argentina kufuatia serikali kuusimamisha uchaguzi wa rais wa chama hicho kinachosimamia soka la Argentina ambao ulipangwa kufanyika Juni 30 huku wakiteuliwa ma-inspectors kuchunguza tuhuma za mapato ya TV ambazo zinalikabili shirikisho hilo.

  Katibu mkuu wa AFA Damian Dupiellet amekiambia kituo kimoja cha redio nchini humo kwamba, bodi ya mkutano wa dharura itaamua kama timu ya taifa ya Argentina itarudishwa nyumbani kutoka Califonia ambako inaendelea na maandalizi kuelekea mashindano hayo.

  “Uchaguzi umesogezwa mbele kwa siku 90 na huenda ukasogezwa mbele kwa siku 90 nyingine tena”, amesema Dupiellet, Katibu Mkuu wa AFA. “Ma-Inspector wawili wameteuliwa kufanya uchunguzi ndani ya AFA. Huku ni kuingilia moja kwa moja masuala ya AFA.”

  FIFA imesimamisha nchi kadhaa miaka ya hivi karibuni kutokana na serikali zao kuingilia masuala ya soka ambazo ni pamoja na Nigeria, Cameroon na Indonesia, huku Dupiellet akiongeza kusema “Tutaomba ufafanuzi toka CONMEBOL na FIFA kufanya upembuzi kama suala hili ni kinyume na kanuni za mashirikisho hayo.

  Taarifa kutoka kitengo cha upelelezi (Inspeccion General de Justicia) ndani ya Wizara ya Haki ya Argentina kuuzuia uchaguzi huo zilithibitishwa na taarifa kutoka tovuti AFA.

  Gazeti la Clarin limeripoti kwamba, matumizi mabaya ya pesa ndani ya AFA ni sababu kubwa iliyopelekea serikali kuingilia na kuupiga 'stop' uchaguzi huo.